Kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, Kiongozi wa Harakati za Kiislamu Nigeria, Seikh Ibrahim Zakzaky (H), amehudhuria Maadhimisho ya Nisfu Sha’aban (Nusu ya Mwezi wa Sha'ban) jijini Abuja kwa mara ya pekee mwaka huu, yakilenga kusherehekea mazazi ya Imam Mahdi (a.j.t.f.s) pamoja na kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwa Sheikh Zakzaky ambayo huangukia tarehe 15 Sha’aban.

6 Februari 2026 - 13:33

Sheikh Ibrahim Zakzaky (H) Ahudhuria na Kuongea na Maelfu wa Waumini Katika Maadhimisho ya Nisfu Sha’aban Abuja, Nigeria

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, mwaka huu Kiongozi wa Harakati za Kiislamu Nigeria, Sheikh Ibrahim Zakzaky (H), amehudhuria moja kwa moja Maadhimisho ya Nisfu Sha’aban yaliyofanyika mjini Abuja.

Maadhimisho hayo yaliandaliwa na Idara ya Masuala ya Kiislamu chini ya uongozi wa Sheikh Ibraheem Yaqoub Zakzaky (H), kwa lengo la kusherehekea mazazi ya Imam wa Mwisho katika Maimamu kumi na wawili wa Shia, Imam Mahdi (a.j.t.f.s), pamoja na maadhimisho ya siku ya kuzaliwa kwa Sheikh Zakzaky ambayo pia huangukia tarehe 15 ya Sha’aban.

Shughuli hizo zilifanyika jioni ya Jumanne, tarehe 15 Sha’aban 1447 Hijria, inayolingana na Februari 3, 2026, katika Ukumbi wa Gadis Event Center, kuanzia saa 9 alasiri, kwa ushiriki wa ndugu na dada wa Kiislamu kutoka ndani na nje ya Abuja.

Sherehe zilianza kwa kikao cha vijana wa Intizarul Imamul Mahdi (a.j.t.f.s), kilichojumuisha maulidi, mihadhara na maonesho yaliyoelezea nafasi na wajibu wa Imam Mahdi (a.j.t.f.s) katika maisha ya Umma.

Baada ya hapo, viongozi wa hafla waliwasilisha wasifu na mashairi maalumu kwa ajili ya Imam Mahdi (a.j.t.f.s) na Jagora Sayyid Zakzaky (H), yakifuatwa na maonesho ya vijana wa Intizarul Imamul Mahdi (a.j.t.f.s) kabla ya kuwasili kwa kiongozi wao.

Kuingia kwa Jagora Sayyid Ibrahim Zakzaky (H) kulipokelewa kwa nashida, qasida na burudani za kiroho kutoka kwa vijana, kisha akatoa hotuba ya kufunga iliyosisitiza subira, utii kwa Mwenyezi Mungu na kusubiri kwa matumaini ujio wa Imam wa Zama (a.j.t.f.s).

Baada ya hotuba yake, Jagora (H) alitoa sadaka kwa kuchinja kwa ajili ya kusherehekea mazazi ya Sahibul-Asr Waz-Zaman (a.j.t.f.s), na hafla ikahitimishwa kwa dua.

Washiriki walimsindikiza Jagora (H) kwa nyimbo za pamoja za “Kulluna Ahmad Ya Aba Ahmad” hadi alipoondoka eneo la tukio, huku wakimshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema ya uhai wake na kumuombea afya, ulinzi na nguvu zaidi katika kuhudumia Umma.

Sheikh Ibrahim Zakzaky (H) Ahudhuria na Kuongea na Maelfu wa Waumini Katika Maadhimisho ya Nisfu Sha’aban Abuja, Nigeria

Your Comment

You are replying to: .
captcha